Kinara wa Kenya shirikisho la mchezo wa Judo Shadrack Maluki, ametangaza azma ya kuwania Urais wa Kamati ya Olimpiki nchini Kenya, NOC-K, kumrithi Dkt Paul Tergat, anayestaafu baada ya kuhudumu kwa kipindi cha mihula miwili.
Maluki, ambaye kwa sasa ni Makamu Rais wa kwanza wa NOC-K, ambapo amehudumu kwa miaka minane, amesema anawania kiti hicho cha Urais akilenga kuboresha maslahi ya wanamichezo, kudumisha uadilifu, uongozi jumuishi, na usimamizi bora wa fedha.
Aidha Maluki, ambaye ni Rais wa Shirikisho la Judo barani Afrika, ameanzisha maafisa, ameanzisha pia kikosi chake cha waaniaji wa nyadhfa mbali mbali kwenye mrengo wake alioupa jina la ‘New Dawn Fresh Nock’.
Mwenyekiti wa riadha ya vijana Barnaba Korir, anawania kiti cha Naibu Rais wa kwanza, huku kinara wa chama cha Magongo Nahashon Randiek, akigombea naibu Rais wa pili.
Kinara wa chama cha Table Tennis Andrew Mudibo,anawakia wadhfa wa Katibu Mkuu, huku mwenzake wa Soft Ball, Francis Karugu, akigombea Katibu Mkuu huku mwenyekiti wa mchezo wa Fencing Fred Chege, akiwania mtunza hazina naye Charles Mose wa shirikisho la Uendeshaji baiskeli akiwania kuwa naibu mtunza hazina.
Bingwa mara mbili wa Olimpiki katika marathon Eliud Kipchoge, anawania kiti cha mwakilishi wanamichezo wakati Lilian Mududa, Joyceline Nyambura na Rais wa chama cha Raga nchini Sasha Mutai, wakiwania viti vya wanachama wa kamati kuu.
Wajumbe 29 kutoka mashirikisho ya michezo nchini yaliyo katika mwavuli wa NOC-K yatapiga kura tarehe 24 mwezi huu.