Madalali wamepata ruhusa kutoka kwa mahakama kunadi mali ya mbunge wa eneo la Mumias Mashariki Peter Salasya ili kulipa deni la shilingi laki 5 analodaiwa na mfanyabiashara Robert Lutta.
Awali, mahakama ilimwagiza Salasya kulipa deni hilo lakini alikosa kufanya hivyo.
Novemba 27, 2023, Hakimu wa Kakamega Gladys Kiama alimwagiza Salasya kulipa deni hilo la shilingi elfu 500, faida yake pamoja na gharama ya kesi, agizo ambalo hakutimiza.
Jukumu la kunadi mali ya mbunge huyo kwa niaba ya mfanyabiashara Robert Lutta, limekabidhiwa kampuni ya madalali ya Armok.
Lutta alimshtaki Salasya mahakamani Oktoba 23, 2023 akidai kumkopesha laki 5 kupitia benki ya KCB na akatoa ushahidi mahakamani.
Salasya kwa upande wake alikana madai hayo na kusema kwamba yeye ndiye alimkopesha Lutta shilingi milioni 1 kupitia kwa mshauri wake wa kisiasa Bernard Kemba.
Hakimu Kiama hata hivyo alipuuzilia mbali madai ya Salasya kutokana na ukosefu wa ushahidi.