Mkuu wa utumishi wa umma siku ya Alhamisi alikutana na makatibu 38 wa wizara katika ukumbi wa Bomas, kujadili utekelezaji kikamilifu wa bajeti ya mwaka wa fedha wa 2023/2024.
Katika mkutano huo, Koskei aliwataka makatibu hao kutumia kwa uadilifu rasilimali za umma na kukabiliana kikamilifu na ufisadi, aliotaja unaenea kwa kiwango kikubwa hapa nchini.
“Wajibu wenu ni kuhakikisha miradi inatekelezwa, kuboresha matumizi ya fedha za umma na kukabiliana ipasavyo na ufisadi,”alisema Koskei.
Aidha, Koskei alitoa wito kwa makatibu hao kuharakisha kulipa madeni yanayodaiwa wizara zao, huku serikali ikijizatiti kuhakikisha hakuna dosari za ukaguzi katika kipindi cha sasa cha fedha.
Aliwahimiza makatibu hao wa wizara, kuwatia moyo wafanyakazi walio katika idara zao na kuepuka mapendeleo katika mchakato wa kuajiri au kuwapandisha vyeo wafanyikazi.
Makatibu hao waliongozwa na katibu katika wizara ya fedha Dkt. Chris Kiptoo na mwenzake wa mipango ya kiuchumi James Muhati.
Dkt. Kiptoo alisema hakuna ushuru utaongezewa wakenya bila mashauriano kufanywa.