Makatibu kutoa uhamasisho kuhusu mpango wa Nyota

Marion Bosire
2 Min Read

Makatibu wa idara mbali mbali za serikali wamejukumiwa na Rais William Ruto kutoa uhamasisho kuhusu mpango wa kuinua vijana kiuchumi uliopatiwa jina NYOTA.

Kiongozi wa nchi aliandaa mkutano na makatibu hao leo katika ikulu ya Nairobi kwa mazungumzo ya kuandaa shughuli hiyo ya uhamasisho katika kaunti zote 47.

Kulingana na Ruto, wameamua kutumia mkakati wa kuhusisha viongozi wote serikalini kuanzisha na kustawisha mpango huo wa kuinua vijana.

“Katika Ikulu ya nairobi, niliandaa mkutano wa ngazi za juu na makatibu wote kujiandaa kwa kuanzishwa kwa mpango wa kuinua biashara za vijana chini ya mradi wa NYOTA.” Alisema Rais.

Katika chapisho lake kwenye akaunti zake rasmi za mitandao ya kijamii, Rais alielezea kwamba Jumatatu Oktoba 6, 2025, makatibu hao watakuwa kwenye kaunti zote kukutana na magavana, wabunge na wawakilishi wadi kuwapa ufahamu kuhusu mpango huo.

Mikutano hiyo ya Jumatatu itatumika pia kuunda mikakati ya utekelezaji wa mpango wa Nyota mashinani.

Serikali inashirikiana na benki ya dunia kwenye mpango huo ambapo kila kijana kati ya vijana 70 waliochaguliwa kutoka sehemu mbali mbali za nchi atapokea shilingi elfu 50, mtaji wa kuanzisha biashara.

“Kwa kuhusisha viongozi kutoka serikali kuu, bunge na serikali za kaunti, mchakato huu utakuwa wazi na jumuishi ili kuhakikisha kila kijana ana fursa ya kunufaika” alisema Rais.

Mpango huo wa shilingi bilioni 5, utanufaisha vijana elfu 100 kote nchini huku Rais akisema kwamba wanawekeza kwa vijana, kufungua fursa na kuendesha ujasiriamali na uvumbuzi kote nchini.

Website |  + posts
Share This Article