Makamishna wa IEBC: Upinzani wadai kuna njama ya kupendelea watu fulani

Martin Mwanje
2 Min Read
Kalonzo Musyoka - Kinara wa chama cha Wiper

Upande wa upinzani ukiongozwa na kinara wa chama cha Wiper Kalonzo Musyoka sasa unadai kuwa kuna njama ya kupendelea watu fulani katika uteuzi wa Mwenyekiti na Makamishna wapya wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC). 

Unaongeza kuwa  njama hiyo ni njia moja ya kutaka kuiba uchaguzi mkuu wa mwaka 2027.

Upinzani sasa unashinikiza kufanywa kwa mazungumzo jumuishi yanayohusisha upande wa serikali na upinzani kabla ya kutangaza waliofanikiwa kuteuliwa kama mwenyekiti na makamishna wa IEBC.

Wiki jana, kamati ya uteuzi ikiongozwa na Dkt. Nelson Makanda ilikamilisha mahojiano ya kumtafuta mwenyekiti mpya wa IEBC katika juhudi za kumtafuta mrithi wa marehemu Wafula Chebukati.

Miongoni mwa wale waliofika mbele ya kamati hiyo ni pamoja na aliyekuwa mwenyekiti wa Tume ya Utekelezaji Katiba (CIC) Charles Nyachae, aliyekuwa Msajili Mkuu wa Idara ya Mahakama Anne Amadi na mwenyekiti wa bodi ya kampuni ya Kenya Power, Joy Masinde Msdivo.

Wengine ni Erastus Edung Ethekon na Francis Kakai Kissinger.

Kwa sasa kamati hiyo inawahoji watu wengine 105 wanaotaka kuwa makamishna wa IEBC.

Akiwahutubia wanahabari akiwa ameandamana na kiongozi wa chama cha DAP-K Eugene Wamalwa na yule wa chama cha PDP Martha Karua, viongozi hao wa upinzani walidai kuwa kuna njama ya kuwateua watu fulani kushika hatamu za uongozi wa IEBC bila kujali ustahili wao.

Upinzani sasa unatoa wito wa kufanywa kwa mazungumzo ya washikadau mbalimbali kabla ya uteuzi wa mwisho wa watakaofanikiwa kuteuliwa kama mwenyekiti na makamishna wa IEBC kufanywa la sivyo uelekee mahakamani kupinga mchakato huo.

TAGGED:
Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *