Maji safi yawaokoa wakazi wa Gafarsa na Iresaboru, Isiolo

Bruno Mutunga
4 Min Read

Wakazi wa vijiji vya Gafarsa na Iresaboru katika Kaunti Ndogo ya Garbatula, Kaunti ya Isiolo sasa wana kila sababu ya kutabasamu, baada ya kukamilika na kufunguliwa rasmi kwa mradi wa kisima cha maji na usambazaji wa maji safi kwa matumizi ya nyumbani, pamoja na bwawa maalum la kunyweshea mifugo.

Mradi huu uliopewa jina la Sustainable Management and Access to Water and Sanitation Services in ASALs Project (SWASAP) umefadhiliwa kwa ushirikiano kati ya Shirika la Maendeleo la Denmark (DANIDA), Water Sector Trust Fund, Serikali ya Kaunti ya Isiolo, na kutekelezwa na Shirika la Msalaba Mwekundu la Kenya (Kenya Red Cross).

Kupitia mradi huo, wakazi wa eneo hili kame sasa wanaweza kupata maji safi na ya kutosha kwa matumizi ya binadamu na mifugo.

Akizungumza na wananchi wa Gafarsa baada ya kufunguliwa kwa mradi huo, Kiongozi wa Masuala ya Mabadiliko ya Tabianchi na Ustahimilivu katika Ubalozi wa Denmark nchini Kenya na Somalia, Tobias Platen, alisifu ushirikiano kati ya wadau mbalimbali wa maendeleo uliofanikisha mradi huo.

Aliwahimiza wananchi kuuthamini na kuulinda mradi huo dhidi ya uharibifu wa aina yoyote, ili uweze kuwanufaisha kwa miaka mingi ijayo. Pia aliwataka waanzishe shughuli endelevu kama vile upandaji miti na bustani za nyumbani ili kuboresha lishe majumbani na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Katibu wa Kaunti ya Isiolo, Dade Boru, ambaye alimwakilisha Gavana Abdi Guyo katika hafla hiyo, alisema kuwa kukamilika kwa mradi huo wa maji sasa kutapunguza kwa kiwango kikubwa magonjwa yanayosambazwa kupita kwa maji machafu, kwani wananchi sasa wana maji safi karibu na makazi yao.

Kabla ya mradi huu, wakazi walilazimika kutembea zaidi ya kilomita saba kutafuta maji kutoka Mto Ewaso Nyiro, maji ambayo hayakuwa salama kwa kunywa kwani walikuwa wakiyatumia pamoja na mifugo na hata wanyamapori kama tembo na nyani.

Chifu Mkuu wa eneo la Iresaboru, Mohamed Diba Wario, alisema kuwa wanawake ambao ndio waliotwikwa jukumu la kutafuta maji walikumbana na hatari nyingi za usalama wakiwa safarini kutafuta rasilimali hiyo muhimu. Changamoto hiyo sasa imetatuliwa kupitia mradi huu.

Afisa Mtendaji Mkuu wa Water Sector Trust Fund, Willis Ombai, alisema kuwa mradi wa SWASAP pia unatekelezwa katika kaunti tano nyingine za Marsabit, Lamu, Tana River, Garissa na Turkana kwa gharama ya jumla ya Shilingi bilioni 1.4, kwa ushirikiano kati ya DANIDA, Water Sector Trust Fund na serikali za kaunti husika.

Alisifu uongozi wa Gavana Abdi Guyo kwa kuhakikisha kuwa Serikali ya Kaunti ya Isiolo ililipa sehemu yake ya bajeti ya mradi mara tu alipoingia madarakani mwaka wa 2022, hatua iliyowezesha mradi wa Isiolo kukamilika kabla ya kaunti hizo nyingine tano.

Wakazi wa kijiji cha Gafarsa, Salesa Forole na Asna Abduba, walieleza kufurahishwa kwao na mradi huo ambao wameutaja kuwa wa kuleta mageuzi makubwa katika maisha yao. Walitaja kupungua kwa magonjwa yanayoletwa kupitia matumizi ya maji machafu na kuondolewa kwa umbali wa kutafuta maji kama mafanikio makubwa.

Hata hivyo, Salesa aliiomba Serikali ya Kaunti pamoja na wadau wa maendeleo kusaidia katika kuchuja chumvi kwenye maji hayo ili yawe bora zaidi kwa matumizi ya binadamu. Pia alitoa wito wa kupanuliwa kwa mtandao wa mabomba ya maji hadi vijiji vya jirani ili wakazi wa maeneo hayo nao wanufaike.

Bruno Mutunga
+ posts
Share This Article