Majambazi waliokuwa na silaha Jumatano alfajiri walivamia na kuiba vifaa vya mamilioni ya fedha katika kampuni moja ya uchimbaji madini, kaunti ndogo ya Rarieda, kaunti ya Siaya.
Majambazi hao waliwashinda nguvu walinzi wa kampuni ya Amlight Resources, ambayo awali operesheni zake zilisimamishwa na mahakama.
Akithibitisha kisa hicho, mkurugenzi wa kampuni hiyo Amos Barasa Mabonga, alisema tukio hilo ni la tano mwaka huu pekee.
Akizungumza akiwa ameandamana na wakili wake Danstan Omari, Mabonga alisikitika kwa hakuna hatua ambayo imechukuliwa, licha ya kuwa wahalifu hao walitambuliwa.
“Shambulizi la kwanza lilikuwa Januari 25, 2024 na kusababisha vifo vya watu wawili. Hadi leo kesi hiyo haijawasilishwa mahakamani,” alishangaa Maboga.
Kulingana na Mabonga, kukosa kuchukuliwa hatua kwa wahalifu hao, kumesababisha mashambulizi zaidi dhidi ya kampuni hiyo.
Wakili Danstan Omari aliwashutumu maafisa wa usalama kwa utepetevu, akiwashutumu kwa uvamizi huo wa mara kwa mara.
“Hii ni kesi ambapo muwekezaji wa hapa nchini anahangaishwa na raia wa kigeni,” alisema Omari.
Alisema atahakikisha waliotekeleza uovu huo wanachukuliwa hatua.