Majaji: Mwilu hakukosea kuteua jopo la kusikiliza kesi ya Gachagua

Martin Mwanje
2 Min Read

Naibu Jaji Mkuu Philomena Mwilu hakukosea katika kuteua jopo la majaji watatu kusikiliza kesi ya kupinga kutimuliwa kwa Naibu Rais Rigathi Gachagua. 

Mwilu mnamo siku ya Jumamosi wiki iliyopita aliliteua jopo la majaji Eric Ogola, Anthony Mrima na Dkt. Freda Mugambi  kusikiliza kesi hiyo.

Katika uamuzi wao, majaji hao wamesema Naibu Jaji Mkuu ana mamlaka kikatba kufanya uteuzi wa majaji kusikiliza kesi panapotokea haja wakati akimsaidia Jaji Mkuu katika utenda kazi wake.

Majaji hao wameapa kuhakikisha wanadumisha utawala wa sheria na kulinda katiba na kupuuzilia mbali madai ya mawakili wa Gachagua kwamba huenda wakaegemea upande mmoja.

Aidha jopo hilo limepuuzilia mbali madai ya mawakili wa Gachagua kuwa Naibu Jaji Mkuu aliandaa kikao Jumamosi iliyopita na kutoa maelekezo pasi ya ufahamu wao wakisema hakuna ushahidi wa kuyathibitisha uliwasilishwa.

Kulingana na majaji hao, maelekezo hayo yalitolewa na Naibu Jaji Mkuu kwa njia ya mtandao.

Hatua hiyo inamaanisha kuwa jopo la majaji hao watatu litaendelea kusikiliza kesi ya kupinga Gachagua kubanduliwa madarakani.

Naibu Jaji Mkuu aliliteua jopo hilo siku moja tu baada ya Mahakama ya Kerugoya Ijumaa iliyopita kutoa agizo la kuzuia kuapishwa kwa Naibu Rais mteule Prof. Kithure Kindiki.

Ni hatua ambayo jana Jumanne ilitifua kivumbi cha kisheria huku mawakili wa Gachagua wakipinga vikali kuteuliwa kwa jopo hilo.

Kulingana na mawakili hao wakiongozwa na Paul Muite, Naibu Jaji Mkuu hana mamlaka ya kuteua jopo hilo, na wajibu huo umetengewa Jaji Mkuu pekee.

Upande wa serikali ukiongozwa na Mwanasheria Mkuu Dorcas Oduor unasema Naibu Jaji Mkuu ana mamlaka ya kuteua jopo hilo na wala hakufanya kosa lolote.

Upande huo unataka maagizo mawili yaliyotolewa yakizuia kuapishwa kwa Prof. Kindiki yafutiliwe mbali ili kupisha kuapishwa kwa mrithi huyo wa Gachagua ambaye alipigwa teke na Bunge la Seneti wiki jana.

 

Share This Article