Maisha Card haina uhusiano na uchaguzi mkuu, yasema serikali

Rahab Moraa
2 Min Read
Katibu katika idara ya uhamiaji, Julius Bitok.

Serikali imekanusha madai kuwa tarehe za mwisho za matumizi ya Maisha Card zina uhusiano na uchaguzi mkuu.

Katika taarifa iliyotolewa leo Jumatatu, Katibu wa Uhamiaji na Utoaji Huduma kwa Watu Julius Bitok amefafanua kwamba siku ya mwisho ya matumizi ya vitambulisho vipya vya Maisha Card  inategemea tu teknolojia ya microchipu iliyopachikwa ndani, sawa na kadi za ATM.

Bitok alisisitiza kwamba Maisha Card ina kifaa kidogo kinachoweza kusomeka kwa mashine, kilicho na vipengele muhimu vya usalama na maelezo ya kibinafsi.

Ufafanuzi huo unafuatia wasiwasi ulioibuliwa na mashirika ya kijamii kuhusu uhalali na muda wa matumizi wa vitambulisho vya kidijitali.

Bitok aliongeza kwamba kuanzishwa kwa Maisha Card kunalenga kuimarisha usalama wa vitambulisho vya kitaifa na kuwiana na viwango vya kimataifa  vya usafiri wa ndege.

Mpango wa Maisha Card ulioanzishwa Februari 23 mwaka huu tayari umepata matumizi makubwa na jumla ya vitambulisho 972,630 kutolewa.

Idadi hii inajumuisha maombi mapya 531,329 na nakala 441,301.

Chini ya mfumo huo mpya, walio na Maisha Card watabadilisha  vitambulisho vyao kila baada ya miaka kumi bila kuhitaji usajili mpya wa kibiometriki.

Hata hivyo, watahitaji kusasisha picha zao za ukubwa wa pasipoti, ili kuonyesha mabadiliko yoyote katika vipengele vya uso baada ya muda.

Kauli ya serikali inalenga kuondoa wasiwasi na kutoa ufafanuzi kuhusu utekelezaji na maelezo ya uendeshaji wa mfumo wa Maisha Card, huku kukiwa na uchunguzi unaoendelea wa umma.

Rahab Moraa
+ posts
Share This Article