Mahakama Kuu imepiga marufuku kwa muda amri iliyotolewa na Rais William Ruto ya kuyataka mashirika yote ya serikali kujiunga na mfumo wa e-Citizen.
Jaji Bahati Mwamuye pia amemzuia Rais Ruto kuwaadhibu wakuu wa mashirika ya kiserikali wanaokaidi agizo hilo kwa kuwabandua afisini.
Rais Ruto alitoa agizo kwa mashirika yote ya kiserikali kutekeleza sheria ya kuhamishia huduma zao zote kwa mfumo wa e-Citezen ifikiapo Januari mosi mwakani.
Mashirika yapatayo 30 bado hajahamishia huduma zake katika mfumo wa e-Citizen.
Mashirika hayo ni pamoja na kampuni ya umeme ya Kenya Power, Mamlaka ya Kudhibiti Bei za Mafuta, EPRA, Mamlaka ya Kusimamia Utendakazi wa Polisi (IPOA) na Chuo Kikuu cha Ulinzi wa Taifa (NDU) miongoni mwa taasisi zingine.
Rais Ruto ameyataka mashirika kuhamia kwenye mfumo wa e-Citizen mara moja.
Serikali inasema mfumo huo umesaidia kuziba mianya ya ufisadi na kuongeza mapato yanayokusanywa na serikali kwa lengo la kufadhili miradi mbalimbali nchini.
Hilo likidhihirika kufuatia tangazo la Mamlaka ya Mapato ya Kenya, KRA kwamba kwa mara ya kwanza imekusanya ushuru wa zaidi ya shilingi trilioni moja.
KRA inasema ilikusanya ushuru wa shilingi trilioni 1.005 kufikia mwisho wa mwezi Novemba mwaka huu.