Mahakama kuu imetoa amri ya kusitisha kwa muda malipo ya karo ya shule za upili za umma kupitia tovuti ya serikali ya eCitizen.
Jaji Chacha Mwita alisema baada ya kusoma maombi ya kesi hiyo, yaliowasilishwa kwake, aliridhika kwamba swala muhimu lilikuwa limeangaziwa.
Kwenye barua ilioandikwa tarehe 31 mwezi Januari mwaka huu, katibu wa elimu ya msingi Belio Kipsang, aliwaaagiza wazazi kulipa karo kupitia tovuti ya serikali ya eCitizen.
Jaji Mwita alisema maagizo zaidi kuhusiana na kesi hiyo yatatolewa tarehe 13 mwezi Februari mwaka huu.
Serikali imekuwa kwenye harakati ya kuweka huduma zote kwenye tovuti ya eCitizen, ili kuimarisha utoaji huduma.
Rais William Ruto alipowahutubia wakenya wanaoishi nchini Japan siku ya Jumanne, alisema sera hiyo mpya inayohitaji karo ya shule kulipwa kupitia tovuti ya eCitizen, inalenga kuondolea mbali malipo ambayo sio halali yanayotozwa na baadhi ya shule.
Alisema serikali imejitolea kuhakikisha inakamilisha uhamisho wa mifumo ya malipo kwa mfumo wa kidijitali.