Mahakama yasimamisha kubinafsishwa kwa mashirika ya serikali

Tom Mathinji
2 Min Read

Mpango wa kubinafsisha mashirika kadhaa ya serikali umesimamishwa kwa muda na mahakama kuu.

Katika kesi iliyowasilishwa na chama cha ODM kinachoongozwa na Raila Odinga, mahakama hiyo ilitangaza kusimamishwa kwa mpango huo wa ubinafsishaji hadi kesi hiyo itakaposikizwa na kuamuliwa.

Jaji Chacha Mwita wa mahakama kuu alisimamisha mpango huo baada ya chama cha ODM kupitia wakili wake Jackson Awele, kusema wananchi hawakupewa muda wa kutosha kutoa maoni yao kuhusu sheria ya ubinafsishaji, kikidai kwamba mashirika hayo huenda yakamilikiwa na kampuni za kibinafsi.

“Agizo limetolewa kusimamisha kutekelezwa kwa sehemu ya 21(1) ya sheria ya ubinafsishaji ya mwaka 2023 hadi February 6, 2024,” aliagiza Jaji Mwita

Chama cha ODM kwenye stakabadhi zilizowasilishwa mahakamani, kilidai kwamba mali ya umma kama vile jengo la mikutano ya kimataifa la KICC, kampuni ya Kenya Pipeline, kampuni ya uchapishaji vitabu ya KLB, na kampuni ya Kenya Seed zinaweza kubinafsishwa baada ya ruhusa kutolewa na wananchi, kupitia kura ya maamuzi.

Waliowasilisha kesi hiyo, walishangazwa ni kwa nini serikali inaharakisha shughuli ya kubinafsisha mali hiyo.

Mnamo tarehe tisa mwezi Oktoba mwaka huu, Rais William Ruto alitia saini kuwa sheria mswada wa ubinafsishaji wa mwaka wa 2023 na kutangaza kuanza kutekelezwa kwa sheria hiyo kuanzia Oktoba 27, 2023.

Wale walioshtakiwa ni pamoja na spika wa bunge la kitaifa, Waziri wa Fedha pamoja na mwanasheria mkuu.

Jaji Mwita aliagiza chama cha ODM kuwasilisha stakabadhi za kesi hiyo kwa wale walioshtakiwa mara moja na kwamba kesi hiyo itasikizwa Februari 6 mwaka ujao.

Share This Article