Mahakama yasema mfumo mpya wa ufadhili wa elimu ya juu ni kinyume cha katiba

Katika uamuzi wake, jaji Chacha Mwita alisema kwamba ni jukumu la serikali kufadhili vyuo vikuu vya umma na kuongeza kwamba kuhamisha jukumu hilo kwa wazazi ni ukiukaji wa Katiba.

Marion Bosire
2 Min Read

Jaji wa Mahakama Kuu Chacha Mwita ametoa uamuzi kwamba mfumo mpya wa ufadhili wa elimu ya juu ni kinyume cha katiba, akisema una ubaguzi kwani wanafunzi wote nchini Kenya wana haki ya kupata elimu.

Mahakama hiyo ilisema pia kwamba ni jukumu la serikali kufadhili vyuo vikuu vya umma na kuongeza kwamba kuhamisha jukumu hilo kwa wazazi ni ukiukaji wa katiba na matarajio halali.

Kulingana na Jaji, ushirikishi wa umma ulikuwa muhimu kabla ya kuanzishwa kwa mfumo huo na kwamba kulikuwa na masuala ya kisheria ambayo yalipaswa kujadiliwa bungeni.

Kesi hiyo iliwasilishwa na Tume ya Haki za Binadamu nchini – KHRC mwaka jana, ikisema kuwa mfumo huo ni kinyume cha Katiba na hauwapatii kipaumbele wanafunzi wanaohitaji msaada.

Waliolalamika dhidi ya mfumo huo walisema umesababisha mkanganyiko katika kuchagua kozi za TVET kwani wanafunzi wanakumbwa na ucheleweshaji kutokana na ukosefu wa maelekezo wazi kutoka huduma ya kusajili wanafunzi wa vyuo vikuu na taasisi nyingine – KUCCPS.

Katika ombi lao kwa mahakama, tume ya KHRC ilisema kwamba mfumo huo wa ufadhili wa elimu ya juu ambao haufanani kwa wanafunzi wote ni wa kimabavu, haujafafanuliwa, ni ghali, ni kinyume cha sheria na ni dhihaka kwa haki ya kupata elimu kama sehemu ya haki za kijamii na kiuchumi.

Walisema pia kwamba washtakiwa wa kesi hiyo walitekeleza mfumo huo kinyume cha sheria na nje ya mamlaka yao na kusababishia madhara maelfu ya wanafunzi wa vyuo vikuu, vyuo anuwai na familia zao.

Mnamo Oktoba 3, 2024, mahakama ilitoa maagizo ya kusimamisha utekelezaji wa mfumo huo hadi kesi ya KHRC, kundi la Elimu Bora na chama cha wanafunzi ikamilike.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *