Mahakama yarejelea kusikiliza kesi ya kutimuliwa kwa Gachagua

Tom Mathinji
1 Min Read
Naibu Rais Rigathi Gachagua.

Mahakama Kuu leo Alhamisi itarejelea vikao vya kusikiliza kesi kuhusu kuondolewa mamlakani kwa Rigathi Gachagua.

Vikao hivyo vitaandaliwa katika ukumbi wa Ceremonial, katika mahakama za milimani.

Jopo la majaji watatu, litajumuisha kesi zote zilizowasilishwa na kushughulikia maswala yaliyoibuliwa na walalamishi kuhusu hatua zilizochukuliwa na bunge la taifa na lile la Seneti.

Hayo yanajiri huku Rigathi Gachagua akipatwa na pigo baada ya Mahakama kuu kutoa uamuzi kwamba naibu jaji mkuu Philomena Mwilu, aliteua ipasavyo jopo la majaji watatu kushughulikia kesi za kumwondoa mamlakani.

Mawakili wa Gachagua wakiongozwa na Paul Muite, walifika mahakamani kulalamika kuwa naibu Jaji Mkuu hana mamlaka ya kutekeleza majukumu ya Jaji Mkuu, na hivyo hatua ya Mwilu kuwateua majaji hao ilikiuka sheria.

Mawakili hao walidai kwamba aliye na uwezo wa kuteua jopo la majaji kusikiza na kuamua kesi hiyo ni jaji mkuu Martha Koome pekee.

Majaji Eric Ogola, Anthony Mrima na Dkt. Freda Mugambi, walitupilia mbali kesi hiyo wakisema haikuwa na msingi, wakithibitisha kuwa naibu Jaji Mkuu anaweza tekeleza majukumu kwa niaba ya Jaji Mkuu.

Mawakili wa serikali wakiongozwa na Prof. Githu Muigai na Tom Ojienda, walikubaliana na uamuzi huo huku wakili wa Gachagua Paul Muite akionyesha ishara za kukata rufaa.

TAGGED:
Share This Article