Mahakama yapiga breki utekelezaji wa mfumo mpya wa ufadhili wa vyuo vikuu

Martin Mwanje
1 Min Read
Mahakama Kuu imesitisha utekelezaji wa mfumo mpya na tata wa ufadhili wa vyuo vikuu nchini.
Hii ni hadi kesi iliyowasilishwa mahakamani kupinga utekelezaji wa mfumo huo isikizwe na kuamuliwa.
Agizo hilo limetolewa na Jaji Chacha Mwita.
Jaji Mwita amesema usikilizaji wa kesi hiyo ulikawia kwa sababu Mwanasheria Mkuu, Waziri wa Elimu na Mamlaka ya Utoaji Nafasi kwa Wanafunzi katika Vyuo Vikuu, KUCCPS zilikosa kuwasilisha mawasilisho yao kwa wakati.
Kesi hiyo iliwasilishwa mahakamani Oktoba 13, 2023 na Tume ya Kutetea Haki za Binadamu, KHRC, Elimu Bora Working Group, Boaz Waruku na vuguvugu la wanafunzi wa vyuo vikuu nchini.
Katika kuiwasilisha kesi hiyo, wote hao walisema mfumo huo ni wa kiubaguzi na unawazuia maelfu ya wanafunzi kupata elimu ya juu.
Kesi hiyo itarejelewa tena Disemba 16, 2024 kwa lengo la kuangazia mawasilisho ya pande husika.
Hayo yanajiri wakati ambapo Rais William Ruto tayari ameteua kamati ya watu zaidi ya 100 ili kuangazia malalamishi ya washikadau kuhusiana na mfumo huo.
Kamati hiyo hasa iliundwa kufuatia upinzani mkali wa mfumo huo kutoka kwa wanafunzi wa vyuo vikuu.
Share This Article