Mahakama moja ya Kabarnet imemwondolea mashtaka Joseph Lesita,ambaye amekuwa akizuiliwa kwa miezi saba iliyopita kwa mashtaka ya madai ya kumbaka msichana mmoja wa umri wa miaka 11 kutokana na ukosefu wa ushahidi.
Lesita alishtakiwa kwa kumbaka mtoto huyo tarehe 28 mwezi septemba mwaka 2023,katika kisiwa cha Kokwa, kata ya Salabani iliyo katika kaunti ndogo ya, Marigat.
Pia alishtakiwa kwa shtaka jingine la kumdhulumu kimapenzi msichana wa umri mdogo. Lesita alikanusha mashtaka hayo mbele ya hakimu mkuu Edwin Mulochi.
Mshtakiwa alikamatwa na walinzi wa ziwa Baringo na kupelekwa katika kituo cha polisi cha Marigat kabla ya kufikishwa mahakamani.
Wakati wa kesi hiyo, afisa wa matibabu katika kliniki ya kaunti ndogo ya Marigat Langat Chirchir,aliwasilisha fomu ya P3 iliyotiwa sahihi na taarifa ya matibabu kama ushahidi ulioonyesha msichana huyo hakubakwa.
Kwenye uamuzi wake,Mulochi alitoa uamuzi kwamba hakukuwa na ushahidi wa kutosha kuonyesha mshichana huyo alibakwa na akaagiza mshtakiwa aachiliwe mara moja.