Mahakama Kuu yafutilia mbali ushuru wa nyumba

Martin Mwanje
1 Min Read

Ushuru wa nyumba wanaotozwa wafanyakazi wanaolipwa mishahara na walio katika ajira rasmi ni kinyume cha katiba. 

Ushuru huo ulianza kutozwa wafanyakazi hao Julai 1, 2023 kufuatia kutekelezwa kwa Sheria ya Fedha ya Mwaka 2023.

Wizara ya Fedha na Mamlaka ya Ukusanyaji wa Mapato Nchini, KRA zimetakiwa kusitisha ukusanyaji wa ushuru huo mara moja.

Jopo la majaji watatu wa Mahakama Kuu katika uamuzi wake leo Jumanne limesema ushuru huo unakosa mpangokazi wa kina wa kisheria kuongoza utozaji wake.

Jopo hilo lilijumuisha majaji David Majanja, Christine Meoli na Lawrence Mugambi.

“Utozaji ushuru dhidi ya watu walio katika ajira rasmi bila kuwajumuisha watu wasio katika ajira rasmi wanaopata mapato bila sababu za kimsingi ni wa kiubaguzi, usiokuwa na mantiki, wa kiholela na dhidi ya katiba,” alisema Jaji Majanja.

Washtakiwa katika kesi hiyo ikiwa ni pamoja na KRA wanataka uamuzi huo kutotekelezwa kwa kipindi cha siku 45 ili kuiwezesha serikali kuangazia suala hilo na kuweka mikakati ya kuwezesha uridhiaji wa uamuzi huo.

Majaji sasa wanatazamiwa kutoa uamuzi kuhusu ombi hilo.

 

 

Share This Article