Mahakama yadumisha hukumu dhidi ya aliyekuwa meneja NSSF

Marion Bosire
2 Min Read

Jamaa mmoja kwa jina Francis Zuriels Moturi aliyehudumu kama meneja wa masuala ya uwekezaji katika hazina ya malipo ya uzeeni NSSF atahudumia kifungo kilichosalia gerezani.

Hii ni baada ya mahakama kuu kutupilia mbali kesi yake ya rufaa ya kupinga kifungo chake cha miaka 14 gerezani alichohukumiwa mwaka 2022 kufuatia kupotea kwa shilingi bilioni 1.2 kutoka kwa hazina ya NSSF.

Jaji wa mahakama kuu Nixon Sifuna alisema kwamba kifungo alichohukumiwa Moturi wa umri wa miaka 70 sasa kiko sawa ikitizamiwa uzito wa mashtaka dhidi yake.

Moturi alipatiwa chaguo jingine na mahakama ya kushughulikia kesi za ufisadi la kulipa faini ya kiwango sawa na mara mbili ya pesa zilizopotea ambayo ni shilingi bilioni 2.4.

Katika kupinga hukumu dhidi yake, Moturi aliambia mahakama kwamba ilikuwa na dosari kwani makosa dhidi yake hayakudhibitishwa ipasavyo na hakukuwa na ushahidi wa kumhusisha na makosa hayo.

Alijaribu kujitetea pia kwa kutumia kosa lililoonekana kwenye stakabadhi ya mashtaka dhidi yake na wakati wa kuhukumiwa ambapo kiwango cha pesa zilizopotea kilikuwa tofauti.

Kosa hilo lilihusisha kampuni ya Discount Securities Limited – DSL ambayo inadaiwa kupokea pesa kutoka kwa NSSF na kuziwekeza kwenye soko la hisa la Nairobi.

Mameneja watayu wa DSL nao walikabiliwa na mashtaka ambapo kila mmoja alihitajika kulipa faini ya shilingi laki nane au kifungo cha miaka 14 gerezani kwa kosa la kula njama ya kulaghai pesa za umma.

watatu hao nao walijaribu kukata rufaa dhidi ya vifungo vyao, rufaa ambazo zilitupiliwa mbali pia na jaji wa mahakama kuu Nixon Sifuna.

Website |  + posts
Share This Article