Mahakama ya Juu leo Jumatatu imeandaa kongamano la kuakisi hatua ilizopiga katika kuwahudumia Wakenya miaka 12 tangu kuasisiwa kwake.
Jaji Mkuu Martha Koome anasema kongamano hilo, lililohudhuriwa na Rais William Ruto na viongozi wengine wakuu serikali, hasa limeangaza umuhimu wa taasisi katika uongozi wa nchi.
“Taasisi ndizo mihimili ya matamanio yetu ya demokrasia,” alisema Jaji Koome wakati akihutubia washiriki wa kongamano hilo ambalo kaulimbiu yake ni ‘Kuakisi na Kutafakari juu ya Utendakazi wa Mahakama ya Juu: Miaka 12 ya Kutetea Katiba.’
“Katika kipindi cha miaka 12 iliyopita, Mahakama ya Juu imetekeleza wajibu wa kuleta mabadiliko yaliyotoa mwelekeo wa sheria nchini Kenya na kuleta maendeleo ya kijamii na kisiasa nchini mwetu. Hukumu za kihistoria za mahakama hiyo zimeleta mabadiliko katika maisha ya kila siku ya Wakenya wakati zikiimarisha kanuni kuu za demokrasia yetu.”
Hata hivyo, miaka 12 baada ya kuasisiwa kwa Mahakama ya Juu, Jaji Koome ambaye pia ni Rais wa mahakama hiyo anasema wamekumbana na changamoto si haba.
Miongoni mwa changamoto hizo ni kutafuta uwiano kati ya maslahi yanayokinzana na matarajio wakati ikihakikisha udumishaji wa sheria.
“Ikizingatiwa mahakama hii hushughulikia kesi zinazohusiana na uongozi, utekelezaji wa mamlaka ya kisiasa na kesi za uchaguzi wa urais, mahakama hii hujipata ikijiingiza katika mizozo inayohusiana na utekelezaji wa mamlaka ya kisiasa. Hii imesababisha mahakama hii kukosolewa kisiasa na kurushiwa mishale ya kisiasa katika chaguzi tatu kuu zilizopita.”
Licha ya changamoto hizo, Jaji Koome ameapa kuwa mahakama hiyo daima itahakikisha utekelezaji wa haki na udumishaji wa utawala wa sheria.
Amewahakikishia Wakenya kwamba kamwe, mahakama hiyo haitatoa maamuzi ya kisiasa.