Mahakama ya Mpeketoni kwa ushirikiano na shirika la kutetea haki za binadamu la waisilamu MUHURI imeanzisha mpango wa kuelimisha wakazi wa kaunti ya Lamu kuhusu haki zao kisheria.
Hakimu mkuu mkazi wa mahakama hiyo Nabwana Pascal anasisitiza kwamba hatua yao imechochewa na jukumu ambalo idara ya mahakama imepatiwa kisheria.
Jukumu hilo ni la kuhakikisha watu wanapata haki kupitia kwa idara hiyo kwa kuwaelimisha na kutagusana nao.
Ushirikiano huo unalenga kuhakikisha kwamba wakazi wa kaunti ya Lamu wamewezeshwa kupitia ufahamu wa haki zao kisheria na njia za kutafuta haki.
Mohamed Skanda kutoka shirika la MUHURI alielezea kwamba watafahamisha wakazi pia kuhusu njia mbadala za kutatua mizozo ambazo zimeidhinishwa na idara ya mahakama.
Alisema pia kwamba wanalenga kuelimisha watu kuhusu urathi na urithi na umiliki wa ardhi ambalo ni suala sugu katika eneo hilo.
Chifu wa eneo hilo Joseph Munene aliunga mkono mafunzo hayo akisema kwamba kesi kuhusu ardhi na ndoa ni nyingi mno na wakazi watakapoelewa namna ya kuzitatua hata yeye atapungukiwa na kazi.
Mhubiri Julius Gachwea kwa upande wake anahisi kwamba mafunzo hayo ya sheria yamewezesha watu kuenda kutafuta huduma za idara ya mahakama wenyewe bila kuhusisha mawakala.