Mahakama Kuu yasimamisha uchaguzi wa mwakilishi wa kiume wa LSK kwenye JSC

Marion Bosire
1 Min Read
Wakili Ishmael Nyaribo

Mahakama kuu imesimamisha uchaguzi wa mwakilishi wa kiume wa chama cha mawakili nchini LSK katika tume ya kuajiri wahudumu wa idara ya mahakama JSC.

Uchaguzi huo ambao ulikuwa umepangiwa kuandaliwa Februari 29, 2024 umesimamishwa baada ya wakili Ishmael Nyaribo kukimbilia mahakama kwa kuachwa nje ya orodha ya wawaniaji wa wadhifa huo.

Jaji John Chigiti ameusimamisha hadi kesi hiyo isikilizwe na kuamuliwa.

Nyaribo anadai kwamba alibaguliwa na hivyo kutojumuishwa kwenye orodha ya wawaniaji hata baada ya kutimiza masharti yote.

Analaumu wahusika kwa kutumia njia zisizo za kikatiba kumfungia nje ya kinyang’anyiro hicho na hivyo kumnyima yeye na wafuasi wake fursa ya kushiriki uchaguzi huo.

Ameshtaki chama cha LSK na bodi ya muda ya uchaguzi ya chama hicho ya mwaka 2024 ambayo wanachama wake ni Rautta Athiambo, Daktari Owiso Owiso, Maria-Goretti Nyariki, Wilkins Ochoki, Serah Esendi Okumu na Esese Harun Ironde.

Walioteuliwa kuwania wadhifa huo Eric Theuri, Michael Wabwile na Omwanza Ombati pia wametajwa kwenye orodha ya wahusika wa kesi hiyo.

Wakili Nyaribo ananyoshea watu hao kidole cha lawama kwa kutoa ilani ya uchaguzi kabla ya kusuluhisha mzozo wa uteuzi wa wawaniaji.

Share This Article