Mahakama Kuu nchini Kenya siku ya Alhamisi, Machi 7 inatarajiwa kuanza kusikiza kesi iliyowasilishwa na chama cha Orange Democratic Movement – ODM kupinga ubinafsishaji wa mashirika 11 ya serikali.
Kesi hiyo iliwasilishwa na ODM kufuatia hatua ya Rais William Ruto kutia saini sheria za ubinafsishaji za mwaka 2023 zinazoruhusu serikali kupiga bei mashirika 11 kwa thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 200.
Kulingana na ODM, mashirika yanayolengwa kubinafsishwa kama vile jumba la KICC, kampuni ya Kenya Pipeline, shirika la Kenya Literature Bureau, na kampuni ya Kenya Seed yanaweza kupata idhini ya kubinafsishwa tu kupitia kwa kura ya maoni kwani ni sehemu ya urithi wa nchi.
Jaji Chacha Mwita alisitisha shughuli ya ubinafsishaji kufuatia kesi hiyo akisema baadhi ya maswali yaliyoibuliwa na ODM yana uzito.