Mageuzi katika sekta ya sukari yanazidi kupiga hatua

Tom Mathinji
2 Min Read
Sekta ya Sukari hapa nchini inazidi kuimarika.

Sekta ndogo ya sukari inazidi kutekeleza jukumu muhimu la kiuchumi na kijamii kila kuchao, huku ikiendelea kupiga jeki sekta ya kilimo na ukuaji wa uchumi wa taifa hili kwa jumla.

Kwa sasa, sekta hiyo inajumuisha kampuni 17 za uzalishaji sukari, ambazo ni uti wa mgongo wa jamii zinazokuza miwa na wakati huo huo kuwafaidi takriban wakulima 300.

Fauka ya hayo, zaidi ya wakenya milioni nane hunufaika pakubwa moja kwa moja na uzalisha sukari, huku wengine wakifaidika kutokana na usambazaji bidhaa na huduma zinazohusiana na uzalishaji huo.

Sekta hiyo huchangia ukuaji wa uchumi wa taifa hili kupitia kubuni nafasi za ajira, ubadilishanaji fedha za kigeni na usambazaji mali ghafi kwa viwanda kadhaa vya kilimo.

Viwanda hivi vinajumuisha vile vya kutengeneza mvinyo, vya kuzalisha umeme na vile vya kutengeneza vinywaji na dawa.

Kampuni hizo 17 za uzalishaji sukari hapa nchini ni pamoja na Chemelil, Muhoroni, Nzoia, South Nyanza, Soin, Miwani, West Kenya (Kabras), Mumias, West Kenya (Olepito), Busia, Butali, Kibos, Sukari, Transmara, West Kenya (Naitiri), Kwale, na West Valley.

Wakati wa kipindi cha kutathmini kilichotekelezwa kati ya mwezi Januari hadi Disemba mwaka 2023, operesheni za kampuni za Miwani na Soin zilikuwa zimesitishwa.

Kampuni ya uzalishaji miwa ya Transmara ilikuwa kifua mbele kwa kuzalisha tani 106,853 za sukari, ukiashiria ongezeko la asilimia 14.1 ikilinganishwa na tani 93,670 zilizozalishwa mwaka 2022.

Kampuni ya Sukari ilichukua nafasi ya pili katika uzalishaji sukari hapa nchini.

Share This Article