Baraza la Magavana (CoG) limeshutumu vikali namna Gavana wa Samburu Lati Lelelit alivyotendewa alipofika katika majengo ya bunge jana Jumatano.
Kwenye taarifa, mwenyekiti wa baraza hilo Ahmed Abdullahi ametaja dhuluma dhidi ya Gavana Lelelit kama kitendo kisichokubalika.
“Kitendo hiki cha kihuni si tu kwamba kinashusha heshima ya afisi ya umma ya Gavana kama Mkuu wa Serikali, bali kinaangazia masuala ya msingi ya kikatiba na utawala wa sheria. Vurugu kama hizo ni ukiukaji mkubwa wa haki za ulinzi ulioelezewa katika Katiba ya Kenya, ambayo inataka kuwepo kwa hadhi ya utu, heshima na uendeshaji wa amani wa masuala ya umma kama kanuni zisizoweza kujadiliwa,” alisema Abdullahi.
Gavana huyo wa Wajir sasa akiutaka uongozi wa bunge kuingilia kati kutoa kinga kwa Magavana kabla ya mambo kwenda mrama hata zaidi.
“Tunatoa wito wa dhati kwa Spika wa Seneti kulaani vikali Maseneta waliohusika katika unyanyasaji huo na kuharakisha mikakati ya kusuluhisha masuala yaliyoibuliwa na Baraza la Magavana dhidi ya baadhi ya wanachama wa Kamati ya Seneti ya Uhasibu wa Fedha za Umma za Kaunti.”
Gavana Abdullahi aliongeza kuwa kitendo alichofanyiwa Gavana wa Samburu ni kosa la kiuhalifu na watawasilisha kesi mahakamani ili wahusika wawajibishwe.
Jana Jumatano, hali ya vuta ni kuvute ilizuka nje ya Bunge la Seneti pale Maseneta walipojaribu kumkamata Gavana Lelelit wakimshutumu kwa kususia wito wa kufika mbele yao.
Ni hali iliyosababisha vurumai kutanda huku Gavana huyo na Maseneta wakionekana kuvutana mashati wakati mmoja kabla ya Lelelit kuingia kwenye gari lake na kuondoka kwa kasi ya umeme.
Akiwahutubia wanahabari katika hoteli moja baada ya kisa hicho, Gavana huyo aliapa kuwashtaki Maseneta waliomdhulumu nje ya Bunge la Seneti.
Mivutano imechacha kati ya Magavana na Maseneta katika siku za hivi karibuni, kiini chake kikiwa matumizi ya kutilia shaka ya fedha za umma katika kaunti mbalimbali.
Ni mivutano ambayo imewafanya Magavana kuapa kususia miito ya kufika Seneti kwa madai ya kufedheheshwa na kutapeliwa.
Kwa upande wao, Maseneta wanasema Magavana watakaokosa kufika mbele yao wataadhibiwa vikali ikiwa ni pamoja na kunyimwa fedha.