Magavana wametishia kusitisha utoaji huduma zote endapo serikali kuu haitatoa pesa katika muda wa siku 30 zijazo.
Wakizungumza wakati wa michezo baina ya kaunti (KICOSCA) katika uwanja wa michezo wa Mumias Sports Complex, Magavana hao wamesema baadhi ya maafisa wa serikali wana njama ya kutatiza ugatuzi kwa kuzinyima kaunti pesa.
Magavana hao wakiongozwa na Gavana wa Kakamega ambaye pia ni mwenyekiti wa kamati ya fedha, mipango na maswala ya uchumi katika Baraza la Magavana (CoG) Fernandes Barasa, wamesema katiba inafaa kuzingatiwa kwa kuhakikisha kuwa kaunti ziko huru kutekeleza majukumu yao.
Aidha wamesema kuwa miradi mingi ya kaunti imekwama kutokana na kucheleweshwa kwa utoaji wa pesa.
Magavana wengine waliohudhuria ni pamoja na Simba Arati (Kisii), Kawira Mwangaza (Meru), George Natembeya wa Tranza Nzoia na Simon Kachapin wa West Pokot.