Magavana watatu kwenye eneo la North Rift wamekubaliana kwamba mifugo wote wawekwe alama, katika hatua mpya ya kukabili kero la wizi wa mifugo na uhalifu mwingine katika eneo hilo.
Magavana Simon Kachapin wa Pokot magharibi, Benjamin Cheboi wa Baringo na Wesley Rotich wa Elgeyo Marakwet waliazimia hayo baada ya kufanya mkutano mjini Iten kuhusu jinsi ya kukabiliana na uhalifu.
Magavana hao waliamua kusitisha uuzaji na uhamishaji wa mifugo kwenye sehemu ambazo zimeathirika na visa vya uhalifu.
Kachapin alisema watashirikiana na serikali ya kitaifa kuhakikisha kuwa mifugo ambao hawajawekwa alama hawahamishwi kutoka sehemu moja hadi nyingine.
Magavana hao tayari wamezindua kamati itakayoongozwa na naibu gavana wa Elgeyo Marakwet Grace Cheserek, kuhakikisha kuwa shughuli ya kuwaweka alama mifugo hao inafanikishwa. Oparesheni inayoongozwa na jeshi dhidi ya wahalifu imekuwa ikitekelezwa kwenye kaunti hizo.