Magavana waonywa dhidi ya kuajiri kiholela

Marion Bosire
1 Min Read
Bw. Twalib Mbarak

Tume ya kupambana na ufisadi nchini Kenya EACC imetoa onyo kwa magavana humu nchini dhidi ya kuajiri watu kiholela katika afisi zao.

Kwenye taarifa kwa magavana Alhamisi Septemba 7, 2023, mkurugenzi mtendaji wa EACC Twalib Mbarak alikumbusha magavana hao kwamba maelekezo ya awali ya tume ya mishahara na mamlaka ya mpito, yaliweka kiwango cha idadi ya maafisa ambao magavana wanaweza kuajiri katika afisi zao.

Mawasiliano hayo kutoka kwa EACC kwa magavana yanafuatia taarifa kwamba baadhi ya magavana wanaunda afisi zisizo halali na kuajiri watu kwa nyadhifa hizo bila kuhusisha bodi za uajiri za kaunti zao.

Mbarak aliwataka magavana ambao wamekiuka maelekezo hayo kurekebisha mambo.

Kila gavana anakubaliwa kuajiri mkuu wa wafanyikazi, mshauri wa masuala ya uchumi, mshauri wa masuala ya siasa, mshauri wa masuala ya sheria, mkurugenzi wa kitengo cha mawasiliano na wasaidizi wa kibinafsi kama, msaidizi wa kibinafsi, katibu wa kibinafsi, mpishi, dereva, mjumbe na mhudumu wa shambani.

Uteuzi wa maafisa hao wa afisi ya gavana ni lazima uidhinishwe na kamati ya uajiri ya kaunti yake.

EACC inaonya kwamba gavana ambaye atakiuka maelekezo hayo ya uajiri wa maafisa katika afisi yake atajukumika iwapo kutapatikana hasara katika matumizi ya fedha afisini kwake kupitia kulipa mishahara isiyostahili.

Website |  + posts
Share This Article