Baraza la magavana limetoa taarifa ya kukatalia mbali nyongeza ya mishahara iliyotangazwa na tume ya mishahara na marupurupu SRC na ambayo inaanza kutekelezwa mwezi huu wa Julai.
Taarifa ya baraza hilo ambayo imetiwa saini na mwenyekiti Anne Waiguru inasema kwamba wamefahamishwa kuhusu arifa ya gazeti rasmi la serikali ya tarehe 9 mwezi Aprili mwaka jana ya SRC.
Arifa hiyo ilitangaza nyongeza ya mishahara kwa maafisa mbali mbali wa serikali kuu wakiwemo maafisa wa magatuzi.
Waiguru ambaye ni gavana wa kaunti ya Kirinyaga anasema wameamua kuomba SRC kutupilia mbali nyongeza hiyo ya mishahara ikitizamiwa hali ngumu ya kiuchumi inayokumba taifa hili.
“Kwa sababu hiyo baraza la magavana linaiomba tume ya SRC kuondoa mara moja nyongeza iliyopendekezwa ya mishahara kwa maafisa wakuu wa serikali za kaunti wakiwemo magavana, manaibu wao na wanachama wa kamati kuu za kaunti.” alisema Waiguru katika taarifa.
Haya yanajiri muda mfupi baada ya walengwa kadhaa wa nyongeza hiyo ya mishahara kujitokeza kuipinga wakati huu ambapo vijana wamekuwa wakiandamana kupinga mswada wa fedha wa mwaka huu.
Maseneta katika kikao chao cha leo walikataa nyongeza ya mishahara sawa na wabunge kadhaa na hata Rais William Ruto ambaye alipendekeza kwamba nyongeza hiyo itathminiwe upya na wizara ya fedha.