Magavana wameelezea kujitolea kwao kushirikiana na washirika wa kimaendeleo katika kuharakisha mabadiliko katika sekta ya afya katika kaunti.
Mwenyekiti wa Baraza la Magavana Anne Waiguru alisema ushirikiano huo utaimarisha utoaji huduma za afya katika kaunti.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mpango wa M-Mama, Waiguru alisema kaunti zimewekeza kwenye nguzo muhimu za sekta ya afya kama wahudumu wa afya, upatikanaji wa dawa muhimu, ongezeko la fedha za kufadhili sekta hiyo kati ya nyingine nyingi.
Waiguru alisifia mpango wa M-Mama akisema utahakikisha hakuna mama atayefariki akijifungua.
Mpango wa M-mama ni ushirikiano kati ya sekta ya umma na ya kibinafsi unaohusisha serikali ya Kenya, serikali ya Marekani kupitia USAID, kampuni ya Vodafone na wakfu wa Mpesa. Ni mfumo wa rufaa za dharura unaohakikisha usafirishaji wa kina mama wanaokaribia kujifungua na watoto waliozaliwa walio na matatizo ya kiafya kwa hospitali zifaazo.
Waiguru alisema kwa kipindi cha miaka 10 iliyopita, serikali za kaunti zimeshirikiana na wadau kuhakikisha upatikanaji wa huduma za afya za ubora wa hali ya juu na nafuu kwa Wakenya wote.
Aliongeza kuwa mpango wa M-Mama ni nyongeza muhimu katika ushirikiano kwenye mipango ya afya ya mama na mtoto nchini.
Waziri wa Afya Susan Nakhumicha alisema kuhakikisha usalama katika kipindi cha ujauzito, wakati wa kujifungua na baada ya kujifungua ni muhimu katika kuafikia mfumo sawa wa afya kwa wote, ambayo ni mojawapo ya ajenda kuu za serikali ya Kenya Kwanza.
Nakhumicha aliongeza kuwa serikali inaridhika kwamba mpango huo utachangia katika kuokoa maisha ya kina mama na watoto.
Kulingana naye, serikali itahakikisha kwamba hakuna atakayeachwa nyuma katika kuafikia mpango wa afya kwa wote kwa sababu za ukosefu wa fedha au vikwazo vya kimazingira.
Alielekeza maafisa katika Wizara ya Afya na katika serikali za kaunti waunde mfumo imara na utakaopatikana wakati wote wa kusafirisha wateja.