Mafuriko yasababisha madhara makubwa Hanang, Tanzania

Marion Bosire
1 Min Read

Watu wapatao 20 wameaga dunia, wengine wamejeruhiwa na wengine hawajulikani waliko kufuatia mafuriko ambayo yamekumba wilaya ya Hanang katika mkoa wa Manyara nchini Tanzania.

Mafuriko hayo yalitokana na mvua kubwa iliyonyesha usiku wa kuamkia Disemba 3, 2023.

Mkuu wa wilaya ya Hanang Janeth Mayanja alitoa taarifa kuhusu janga hilo akisema shughuli za kuokoa waliokwama kwenye mafuriko zilikuwa zikiendelea huku akishauri watu kutahadhari.

Kamanda wa polisi katika mkoa wa Manyara George Katabazi alielekea eneo la Hanang kujionea hali ilivyo na kushirikisha shughuli ya uokoaji.

Maji mengi ya mafuriko yaliingia kwenye nyumba za watu wa eneo hilo yakiwa yamebeba miti iliyong’oka na mawe makubwa, vitu ambavyo vilisababisha kuharibiwa kwa nyumba kadhaa.

Yanasemekana kutoka kwenye mlima Hanang.

Mayanja alitangaza kwamba miili ya waathiriwa imehifadhiwa katika makafani ya hospitali ya Tumaini.

Barabara nyingi za eneo hilo zimeharibiwa na hazipitiki ikiwemo ile ya kutoka Sindiga kuelekea Babati.

Mashirika ya kushughulikia barabara na miundombinu kama TANROADs na TARURA yanatekeleza juhudi za kurejesha barabara hizo katika hali nzuri.

Share This Article