Serikali imetangaza kafyu ya siku 30 katika maeneo 12 kaunti ya Tana River, yakitajwa kuwa hatari na yasiyo na usalama.
Hayo yanajiri baada ya jamii mbili kuzozania eneo la maji na kusababisha vifo vya watu 14 hadi kufikia sasa.
Waziri wa usalama wa kitaifa Prof. Kithure Kindiki kupitia gazeti rasmi la serikali, alisema kafyu hiyo itaanza kutekelezwa leo Ijumaa saa kumi na mbili na nusu jioni.
Maeneo yanayoathiriwa na kafyu hiyo ni pamoja na Madogo, Areri, Saka, Sala, Mororo na Mbalambala katika kaunti ndogo ya Bangale. Maeneo yaliyoathiriwa kaunti kaunti ndogo ya Tana Kaskazini ni pamoja na Hirimani,Hosigo, Dukanotu, Chewele, Bura na Nanighi.
Kindiki alisema kuwa uamuzi huo uliafikiwa baada ya kushauriana na baraza la kitaifa la usalama ili kushughulikia wasiwasi wa kiusalama kwenye eneo hilo.
Wakati huo huo, Inspekta Jenerali wa polisi Douglas Kanja, naye ametangaza marufuku dhidi ya kumiliki silaha kwenye maeneo hayo, akiwataka wakazi wasalimishe bunduki zote katika vituo vya polisi wakati wa mchana kwa ili zihifadhiwe.
Wakazi kadhaa wa maeneo ya Nanigi, Anole na Vango wametoroka kwa kuhofia mashambulizi.