Shirika la Maendeleo ya Wanawake, MYWO limeitaka serikali na upinzani kuzungumza ili kuepusha maafa na uharibifu wa mali unaoletwa na maandamano ambayo yamekuwa yakiitishwa na upinzani.
Akihutubia wanahabari leo Jumanne, mwenyekiti wa MYWO Rahab Mwikali amesema ni wakati mwafaka kwa pande zote kuweka maslahi ya Wakenya mbele.
“Sisi kama kina mama, tunahuzunika kuona hali ilivyo nchini. Wiki iliyopita pekee, tulipoteza watu 23 kutokana na maandamano na hatutaki kupoteza maisha zaidi,” alisema Mwikali.
“Sisi tunamwomba aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga asitishe maandamano na amuite Rais kwa meza ya mazungumzo.”
Mwikali pia amemwomba Rais kushughulikia kwa dharura gharama ya juu ya maisha huku Wakenya wengi wakiendelea kutaabika.
Kwa upande wake, mwenyekiti wa zamani wa MYWO Ziporah Kitony ametaja hali ya sasa nchini kuwa inayotishia ukuaji wa nchi na uchumi.
Matamshi yao yanajiri siku moja kabla ya muungano wa Azimio One Kenya kufanya maandamano ya kitaifa kuishinikiza serikali kupunguza gharama ya maisha.