Msanii wa muziki nchini Tanzania Hamad Ally maarufu kama Madee, ameondolewa marufuku na Baraza la Sanaa la Taifa, baada yake kutekeleza mahitaji.
BASATA ilichapisha barua ambayo inaonyesha kwamba mwimbaji huyo amelipa faini na kubadili wimbo uliosababisha hatua ichukuliwe dhidi yake.
Disemba 14, 2023 BASATA ilichukua hatua ya kumpiga marufuku Madee na kumtoza faini ya shilingi milioni 3 pesa za Tanzania.
Marufuku ilikuwa idumu hadi pale ambapo angetekeleza mahitaji ya BASATA kulingana na sheria zake za maadili ya kijamii.
Kando na kuondolewa marufuku, Madee amekubaliwa kuutumia wimbo huo wake ambao sasa ameubadilisha. Awali alikuwa ameupa mada ya “Nakojoa Pazuri”.
Sasa anaweza kuchapisha wimbo huo hata kwenye majukwaa ya muziki mitandaoni.
BASATA imetoa onyo kali kwa wasanii ikisema ukiukaji wa maadili katika shughuli za Sanaa hautavumiliwa na kuwataka wafanye kazi zao kwa kuzingatia mwongozo wa maadili wa BASATA kwa mwaka 2023.
Wasanii wengine ambao wamejipata katika hali sawia katika siku za hivi karibuni ni pamoja na Whozu, Mbosso na Billnass kufuatia wimbo wao kwa jina “Ameyatimba Remix”.