Madarasa ya wanafunzi wa Gredi ya 9 kuwa tayari kabla ya shule kufunguliwa, asema Waziri Ogamba

Martin Mwanje
2 Min Read
Julius Ogamba - Waziri wa Elimu

Waziri wa Elimu Julius Ogamba ameelezea matumaini kuwa ujenzi wa madarasa yatakayotumiwa na wanafunzi wa Gredi ya 9 utakamilika kabla ya kufunguliwa kwa shule mapema mwezi Januari mwakani.

Amesema serikali inajenga madarasa 11,000 yatakayotumiwa na wanafunzi hao.

Kulingana na Waziri Ogamba, ujenzi huo ulianza mwezi Julai, 2024 na unatarajiwa kukamilika kabla ya shule kufunguliwa.

Aidha, amesema Wizara yake inashirikiana na Hazina ya NG-CDF kujenga madarasa mengine 6,800.

Aliyasema hayo jana Jumatano jioni wakati wa mkutano wa mashauriano na washikadau juu ya CBC ulioandaliwa katika Taasisi ya Utayrishaji wa Mtaala nchini, KICD, jijini Nairobi.

Matamshi yake yanajiri wakati baadhi ya washikadau wametilia shaka ikiwa ujenzi wa madarasa hayo utakamilika kabla ya shule kufunguliwa mwezi ujao.

Wakati huohuo, Waziri Ogamba amesema takriban shilingi bilioni 85.5 zimetumiwa kufadhili mtaala wa umilisi, CBC, katika shule za msingi katika kipindi cha miaka 9 iliyopita.

Amesema fedha hizo zilitumiwa kati ya kipindi cha miaka ya fedha 2016/2017– 2024/2025.

 Waziri Ogamba amesema kiasi cha fedha ambazo zimewekezwa katika shule za sekondari ya chini, JSS katika kipindi cha miaka ya fedha ya 2023/2024- 2024/2025 ni bilioni 61.66.

Kulingana naye, shilingi bilioni 310 zimetumiwa kufadhili masomo katika shule za upili katika kipindi cha miaka mitano iliyopita ya fedha.

‘‘Ufadhili wa serikali wa masomo ya shule za upili katika kipindi cha miaka mitano iliyopita ya fedha kilikidhi mahitaji ya wanafunzi 19,084,644’’ ameongeza Waziri huyo.

Serikali hutenga shilingi 1,420 kwa kila mwanafunzi wa Gredi ya 1-6 kila mwaka, shilingi 15,042 kwa shule za JSS na shilingi 22,244 kwa shule za upili.

 

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *