Madaktari kupitia chama chao cha madaktari, wataalamu wa dawa na meno KMPDU, wametoa ilani ya wiki mbili ya mgomo katika hospitali ya kitaifa ya Kenyatta.
Chama hicho kinalaumu usimamizi wa hospitali ya Kenyatta kwa kubagua baadhi ya wahudumu kwa kuwalipa mshahara nusu ya ule wanaopata wengine.
Viongozi wa chama cha KMPDU wanasema hali si hali katika sekta ya afya kwenye magatuzi na wakatoa notisi kwa serikali za kaunti za Busia, Kakamega, Machakos, Kiambu, Garissa na Nakuru. Wiki ijayo madaktari wa kaunti za Kakamega na Busia wanapanga kuandaa mgomo baridi kutokana na kile ambacho chama hicho kinataja kuwa utunzaji mbaya wa wahudumu wa afya.
Wahudumu wa afya katika kaunti ya Machakos nao wametoa ilani ya siku saba ya mgomo huku serikali ya kaunti ya Garissa ikilaumiwa kwa kusimamisha mishahara ya wahudumu wa afya kinyume cha sheria zilizopo za utendakazi.
Serikali ya kaunti ya Nakuru nayo imekuwa ikielekezewa lawama kwa kuwafuta kazi madaktari 500.
Chama cha KMPDU pia kinataka madaktari waongezewe mishahara kuambatana na ongezeko la gharama ya maisha.
Kuhusu hazina ya kitaifa ya bima ya afya NHIF, madaktari wanataka mbinu za kuhakikisha uwajibikaji ziwekwe kabla ya wakenya kuongezewa kiwango cha michango ya kila mwezi kwa hazina hiyo.