Madaktari waapa kulemaza huduma hospitalini wiki ijayo

Dismas Otuke
1 Min Read

Chama cha Madaktari nchini, KMPDU kimetishia kusitisha huduma katika hospitali za umma kote nchini kuanzia Jumapili ijayo kutokana na kile kinachodai kuwa kupewa ahadi hewa na serikali.

Katibu Mkuu wa KMPDU Dkt. Davji Atellah akiwatubia madaktari leo Jumatatu, amesema serikali haikutekeleza ahadi yake na maafikiano yaliyosababisha kusitishwa kwa mgomo wa awali.

Dkt. Atellah ameahidi kuwa watalemaza huduma za matibabu katika hospitali zote za umma kuanzia Jumapili usiku wa manane, Disemba 22 hadi pale serikali itakapotimiza matakwa yao.

Madaktari wa KMPDU walisitisha mgomo wa kitaifa wa siku 56  mapema mwezi Mei mwaka huu baada ya kuafikiana na serikali ya kitaifa na zile za kaunti kuhusu masuala tata.

Miongoni mwa masuala hayo ni pamoja na uboreshaji wa mazingira ya utendakazi, kupandishwa vyeo, kuongezwa mishahara na suala tata la malipo ya madaktari wanagenzi.

KMPDU inataka madaktari wanagenzi walipwe mshahara wa shilingi 206,000 kwa mwezi kama ilivyokubaliwa kwenye mkataba wa maelewano kati ya serikali na chama hicho.

Kwa upande wake, serikali inasema inasema inaweza tu kuwalipa madaktari hao mshahara wa shilingi 70,000 kwa mwezi, mshahara unaopingwa na serikali.

Suala hilo lingali mahakamani ila serikali na vyama vya matabibu zimetakiwa kushiriki mazungumzo ya kufikia makubaliano juu ya mvutano huo.

TAGGED:
Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *