Madaktari kaunti ya Migori warejea kazini

Tom Mathinji
1 Min Read
Hospitali ya Rufa kaunti ya Migori.

Madaktari katika kaunti ya Migori wamerejea kazini baada ya mazungumzo kati yao na serikali ya kaunti kufanikiwa. 

Gavana wa kaunti hiyo Ochilo Ayacko, akithibitisha hayo, alitoa wito kwa madaktari kutii agizo la mahakama na kurejea kazini huku mazungumzo yakiendelea.

Alisema serikali ya kaunti ya Migori imetimiza matakwa saba kati ya tisa yaliyowasilishwa na madaktari hao, huku akidokeza kuwa ni muhimu kwa madaktari kurejea kazini kwa maslahi ya afya ya umma.

Ayacko alikariri kujitolea kwa serikali ya kaunti katika kushirikiana na wahudumu wa afya ili kulainisha upatikanaji wa huduma za afya katika kaunti hiyo.

Aliwahimiza madaktari  kote nchini kuwaepushia mateso Wakenya wanaotafuta huduma za afya wanapopigania haki zao.

“Msikome kutekeleza majukumu yenu kwa umma kwa kuwa matakwa yenu hayajatekelezwa, tuendelee kuzungumza tunapozingatia hadhi na maisha,” alisihi Ayacko.

Share This Article