Madai ya ubaguzi: Mameneja wa BAT wahojiwa na bunge

Marion Bosire
3 Min Read
James Gakuya, mwenyekiti wa kamati ya bunge kuhusu biashara

Kamati ya Biashara, Viwanda na Ushirika inaendeleza uchunguzi wake kuhusu madai kwamba kampuni za kimataifa zinabagua wawekezaji wa humu nchini wa sekta ya uchukuzi na usafirishaji.

Jana wabunge wanachama wa kamati hiyo wakiongozwa na mwenyekiti James Gakuya wa Embakasi Kaskazini walikutana na mameneja wakuu wa kampuni ya British American Tobacco – BAT Kenya kujadili madai ya kubagua wasafirishaji hao wa humu nchini.

“Je, ni kweli kwamba mnaingia kwenye mikataba ya kipekee na mashirika ya kimataifa kama lenu katika masuala ya usafirishaji?” aliuliza Gakuya wakati wa mkutano na maafisa wa BAT wakiongozwa na mkurugenzi mkuu Crispin Achola.

Mkurugenzi huyo wa BAT Kenya alikanusha madai hayo na kuihakikishia Kamati hiyo kwamba kampuni hiyo ya kimataifa inashughulikia kwa haki wasambazaji wa nhumu nchini na wa kimataifa.

Achola alielezea kwamba kati ya wasambazaji 20 waliopatiwa kandarasi na BAT Kenya, asilimia 70 wa humu nchini huku asilimia 30 wakiwa wa kimataifa.

Wasambazaji wa kimataifa alisema huwa wanatoa huduma za ugavi wa mwisho hadi mwisho kama uhifadhi wa bidhaa, kusafisha, kusambaza na huduma za usafiri.

Mnamo Machi 6, Kamati hiyo ilifanya kikao na wawakilishi wa muungano wa wasafirishaji nchini yaani Kenya Transporters Association (KTA) ambao waliomba bunge liingilie kati mzozo unaoendelea kati ya wasafirishaji wa ndani na kampuni za kimataifa.

Mwenyekiti wa KTA Newton Wang’oo alidai kuwa kampuni za kimataifa zinapendelea kushirikiana na kampuni ya kimataifa katika sekta ya uchukuzi, jambo ambalo alisema ni biashara isiyo ya haki.

Wiki iliyopita, Naibu Mwenyekiti wa Kamati hiyo Marianne Kitany (Aldai) aliagiza Mamlaka ya Ushindani ya Kenya kuchunguza madai hayo.

Keitany wakati wa mkutano na Adan Roba mkurugenzi mkuu wa mamlaka ya ushindani alimwagiza afanye uchunguzi zaidi kuhusu tuhuma hizo.

Alisisitiza kwamba uchunguzihuo ufanywe katika sekta nyingine za uchumi mbali na ile ya uchukuzi na usafirishaji.

Kamati hiyo wiki iliyopita pia ilishauriana na maafisa wakuu wa kampuni mbili za kimataifa zinazofanya kazi nchini Kenya.

Mkurugenzi Mkuu wa kampuni ya Unilever Kenya Luck Ochieng na Afisa Mkuu wa Fedha wa kamouni ya Nestlé Kenya Limited Gibson Singen walikanusha madai ya ukosefu wa haki wakisema kampuni zao hushirikiana vyema na wasafirishaji wa humu nchini.

Share This Article