Mhubiri tata Paul Mackenzie na washtakiwa wenzake 29 wamekanusha mashtaka ya mauaji ya watoto 191 ambao miili yao ilifukuliwa kutoka kwenye msitu wa Shakahola.
Washukiwa hao walikana mashtaka hayo mbele ya jaji Mugure Thande katika mahakama kuu huko Malindi.
Mmoja wao kwa jina Evans Sirwa hata hivyo hakuwepo mahakamani kwa ajili ya kosomewa mashtaka kwa sababu alipatikana kutokuwa katika hali nzuri kiakili.
Kesi ya mauaji dhidi ya Mackenzie na wenzake ilicheleweshwa kwa muda wa wiki mbili ili kutoa fursa ya wote kufanyiwa uchunguzi wa kiakili ili kuona iwapo wako sawa.
Kiongozi huyo wa kanisa la Good News International aliamuru wafuasi wake kufunga kula na kunywa ili waweze kufika mbinguni kumwona Mungu.
Baada ya vitendo vyake kugundulika, maafisa wa serikali walitumia muda wa miezi kadhaa kufanya uchunguzi na ufukuzi wa miili kwenye msitu wa Shakahola.
Miili zaidi ya 400 ilifukuliwa na kulingana na uchunguzi wengi walikufa kwa kukosa chakula na maji huku wengine wakinyongwa.
Baadhi ya wafuasi wa Mackenzie ambao bado walikuwa wanatekeleza amri yake waliokolewa wakati wa uchunguzi huo huku wakiwa wamekonda sana.
Wafuasi wa mhubiri huyo walikatazwa kupeleka wanao shuleni kwani kulingana na Mackenzie taasisi za elimu zilikuwa za kishetani na hilo ni kojawapo ya mashtaka dhidi yake na washukiwa wenza.
Kosa hilo ni kunyima watoto haki ya kupata elimu.
Kanisa lake tayari limetangazwa na serikali kuwa kundi la uhalifu uliopangwa.