Serikali imewaagiza wasimamizi wote wa mitihani ya kitaifa kuhakikisha kila mwanafunzi anafanya mtihani wa darasa la nane KCPE.
Kupitia kwa taarifa, waziri wa elimu Ezekiel Machogu, alisema wizara yake imepokea habari kwamba baadhi ya shule hazikuwasajili wanafunzi kufanya mtihani wa kitaifa wa darasa la nane KCPE, akisema kuwa hatua kali zitachukuliwa dhidi ya waliohusika.
Machogu aliwaagiza wanafunzi wote ambao hawakusajiliwa kufanya mtihani wa KCPE kufika katika shule walikosomea ili kufanya mtihani huo.
Akisikitikia hali hiyo, Machogu alisema hatua hiyo ya kutowasajili wanafunzi kufanya mtihani wa kitaifa ni kosa kubwa na ambalo huwatatiza wanafunzi kimawazo.
“Kwa kuwa huu ndio mtihani wa mwisho wa, wanafunzi hawatafukuzwa katika vituo vya kufanyia mitihani kwa misingi kwamba hawajasajiliwa,”alisema Machogu.
Mtihani wa darasa la nane KCPE na tathmini ya gredi ya sita imeanza kote nchini Jumatatu asubuhi, na itakamilika siku ya Jumatano.
Wanafunzi 1,415,315 wanatarajiwa kufanya mtihani wa KCPE huku wanafunzi 1,282,574 wakifanya mtihani wa KPSEA.