Mabalozi wateule waanza kupigwa msasa na bunge

Martin Mwanje
2 Min Read
Catherine Kirumba Karemu aliyeteuliwa kuhudumu kama balozi wa Kenya nchini Uingereza

Usaili wa watu walioteuliwa na Rais William Ruto kuhudumu kama mabalozi katika nchi mbalimbali mwezi jana umeanza leo Alhamisi asubuhi. 

Wa kwanza kufika mbele ya kamati ya bunge inayoendesha usaili huo alikuwa ni Catherine Kirumba Karemu aliyeteuliwa kuwa balozi mpya wa Kenya nchini Uingereza.

Ikiwa ataidhinishwa kushikilia wadhifa huo, basi Karemu atachukua nafasi ya Manoah Esipisu.

Akihojiwa, Karemu ameelezea utayari wake wa kuchapa kazi kwa bidii ya mchwa ikiwa uteuzi wake utaidhinishwa na kufichua kwamba thamani ya utajiri wake ni shilingi milioni 250.

Katika uteuzi huo wa watu 43 watakaohudumu kama mabalozi na manaibu balozi katika nchi mbalimbali za kigeni, baadh ya wanasiasa walinufaika pakubwa.

Miongoni mwao ni aliyekuwa mbunge wa Nyando Fred Outa ambaye aliteuliwa kuwa balozi wa Kenya nchini Misri.

Naibu Gavana wa zamani wa kaunti ya Kisii Joash Maangi kwa upande mwingine aliteuliwa kuwa balozi wa Kenya nchini Uganda.

Aliyekuwa Seneta mteule Petronila Were aliteuliwa kuhudumu kama naibu balozi wa Kenya nchini Ethiopia.

Kwa upande mwingine, nafasi ya Balozi Lazarus Amayo nchini Marekani itachukuliwa na David Kiplagat Kerich ikiwa uteuzi wake utaidhinishwa na bunge.

Wengine walioteuliwa kuhudumu kama mabalozi ni Lilian Tomitom (Zambia), Vincent Mogaka Kemosi (Ghana, Profesa Anne Kisaka Nanguli (Senegal), Luteni Jenerali Peter Mbogo Njiru (Pakistan), Timothy Kaluma Mcharo (Algeria) na Caroline Kamende Daudi (Canada).

Jessica Muthoni Gakinya aliteuliwa kuhudumu kama Balozi wa Kenya nchini Morocco, Halima Yussuf Mucheke (Uholanzi), Everylyne Mwenda Karisa (Cuba), Dkt. Peter Mutuku Mathuki (Urusi), Moi Lemoshira (Japan), Kenneth Milimo Nganga (UAE), Luteni Jenerali Jonah Mwangi (Iran) na Abdi Aden Korio (Oman).

Aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano nchini, CA Ezra Chiloba aliteuliwa kuhudumu kama mkuu wa ubalozi mdogo wa Kenya mjini Los Angeles nchini Marekani.

Majina ya walioteuliwa yamepelekwa bunge ili kupigiwa msasa kabla ya Rais Ruto kuwateua rasmi kuhudumu katika nyadhifa hizo ikiwa uteuzi wao utaidhinishwa na bunge.

Share This Article