Mabalozi kutoa ripoti kila mwezi kuhusu utangazaji wa bidhaa za Kenya

Marion Bosire
2 Min Read

Naibu Rais Rigathi Gachagua amesema kwamba mabalozi wa Kenya watakuwa wakitoa ripoti ya kila mwezi kuelezea hatua walizochukua kutangaza bidhaa za Kenya katika nchi wanakohudumu.

Gachagua ambaye alikuwa akizungumza kwenye mkutano na Wakenya wanaoishi na kufanya kazi nchini Italia, alisema kuanzia sasa, jukumu kuu la mabalozi ni kutangaza bidhaa za Kenya na kuhakikisha wasifu wa kibiashara wa nchi hii unaimarika ulimwenguni, kando na majukumu mengine ya kibalozi.

Alisema wawakilishi hao wa serikali ya Kenya ughaibuni watapatiwa taarifa hitajika ili waweze kulainisha malengo yao yaangazie mauzaji ya bidhaa za Kenya.

Kulingana naye, serikali ya Kenya Kwanza inahakiki majukumu ya mabalozi ili sehemu kubwa ya kazi yao ambayo ni sawa na kiwango cha asilimia 70 iwe kutangaza chai, kahawa na bidhaa za matunda na mboga kutoka Kenya.

Gachagua alisema serikali inabadili majukumu ya mabalozi kutoka yale ya awali ya kuhudhuria mikutano, na sasa watakuwa wanaelezea kila mwezi mikutano ambayo wamefanya ya kutangaza bidhaa za Kenya na mikataba waliyoafikia kuhusu bidhaa hizo.

Aliongeza kuwa mabalozi hao hivi karibuni watahitajika kutia saini mikataba ya miaka miwili ya kutekeleza jukumu hilo jipya.

Rigathi aliwapa changamoto Wakenya wanaoishi nchini Italia washirikiane kwa karibu na idara ya serikali ya masuala ya ughaibuni ambayo ilibuniwa kushughulikia mambo yao.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *