Maandamano yashuhudiwa LA huku wanajeshi wakitumwa kutuliza hali

Wakazi wa eneo hilo waligeukia maandamano kama njia ya kulalamikia uvamizi wa maafisa wa uhamiaji ambao wamekuwa wakikamata wahamiaji haramu

Marion Bosire
2 Min Read

Maandamano yameshuhudiwa katika eneo la mji wa Los Angeles nchini Marekani na Rais Donald Trump ametuma wanajeshi wa kikosi cha National Guard kutuliza hali.

Wakazi wa eneo hilo waligeukia maandamano kama njia ya kulalamikia uvamizi wa maafisa wa uhamiaji ambao wamekuwa wakikamata raia wa kigeni walioko katika eneo hilo wasio na stakabadhi za kuhalalisha uwepo wao nchini Marekani.

Vurugu hizo zilizozuka karibu na jengo la mahakama la Edward R Roybal, gereza la Metropolitan na barabara ya 101 Freeway zilijiri kwenye siku ya tatu ya msako wa wahamiaji haramu ambapo wengi tayari wamekamatwa.

Maafisa wa polisi wa Los Angeles au ukipenda LAPD, wale wa mashinani wa Los Angeles, wanaoshika doria barabarani huko California wanashirikiana na wale wa kitengo cha National Guard waliotumwa na Trump kutuliza hali.

Watekelezaji hao wa sheria wamekuwa wakitumia risasi za mipira na gesi za kutoza machozi kujaribu kutawanya waandamanaji huku wakitangaza eneo la Downtown Los Angeles kuwa lisilo la mikutano ya hadhara.

Video zilizosambaa za tukio hilo la Jumapili usiku kulingana na saa za Marekani zinaonyesha makundi mbali mbali ya raia yakikabiliana na maafisa hao wa usalama.

Hata hivyo video zisizo sahihi zilisambaa awali kuonyesha tukio hilo. Video hizo za maandamano ya mwaka 2020 ya kulalamikia mauaji ya George Floyd, zimesambazwa mitandaoni na watu tajika akiwemo Seneta wa Texas Ted Cruz.

Website |  + posts
Share This Article