Maafisa zaidi wa uhamiaji kupelekwa mipakani kudhibiti ugonjwa wa Mpox

Tom Mathinji
1 Min Read

Maafisa zaidi wa uhamiaji watapelekwa katika maeneo ya mipakani, kupiga jeki juhudi za kuzuia kuenea kwa ugonjwa wa Mpox hapa nchini, hayo ni kulingana na katibu katika idara ya uhamiaji Julius Bitok.

Kwa mujibu wa Bitok, maafisa hao wanatarajiwa kushirikiana kwa karibu na maafisa wa afya na wale wa asasi zingine za serikali, kuhakikisha wageni wote wanakaguliwa ipasavyo.

“Wale watakaotumwa katika mipaka ya ardhini,angani au baharini, watajiunga na maafisa wengine kutoka idara ya usalama, kilimo, wale wa ukusanyaji ushuru na wengine waliojukumiwa kulinda mipaka ya taifa hili dhidi ya wageni ambao wameambukizwa,” alisema Bitok.

Katibu huyo aliyasema hayo wakati wa sherehe ya kufuzu kwa maafisa wapya 300 wa uhamiaji, katika taasisi ya serikali ya Kabarnet kaunti ya Baringo.

Bitok alisema wizara yake imo mbioni kutekeleza mageuzi makubwa ya kuipa idara ya uhamiaji sura mpya, kinyume na ilivyokuwa awali, kwa sababu ya visa vya ufisadi.

Maafisa hao waliopokea mafunzo ya wiki tano kuhusu taratibu za uhamiaji, usalama, ujasusi, mawasiliano, itifaki na afya, pia watapelekwa katika afisi ya pasipoti, leseni na idara zingine za utoaji huduma.

Share This Article