Tume ya Maadili na Kukabilina na Ufisadi Nchini (EACC) imewakamata maafisa wanne wa Hazina Kuu kwa madai ya kushiriki ufisadi.
Washukiwa hao wanajumuisha Maafisa Wakuu na makarani, wanashtumiwa kuongoza genge ambalo limekuwa likiwahadaa wananchi ambao wamekuwa wakitafuta huduma kwenye Hazina Kuu.
Uchunguzi wa EACC ulibainisha kwamba washukiwa hao walipokea hongo kupitia akaunti ya simu ya paybill, ambayo ilikuwa imesajiliwa na mmoja wa maafisa hao.
Kwa mujibu wa tume hiyo, akaunti hiyo ya paybill ilikuwa imepokea takriban shilingi milioni 10.5 kwa muda wa miaka miwili iliyopita.
“Washukiwa hao wanahojiwa katika Makao Makuu ya ya EACC na baadaye watazuiliwa katika kituo cha polisi cha Kilimani, huku uchunguzi ukiendelea,”alisema Afisa wa Mawasiliano wa tume hiyo Stephen Karuga kupitia kwa taarifa.
Tume imeelezea kujitolea kwake kukabiliana na ufisadi katika Taasisi za Umma.