Maafisa wa utawala watakiwa kuhakikisha utekelezaji wa miradi ya serikali

Martin Mwanje & DPCS
1 Min Read

Naibu wa Rais Rigathi Gachagua ametoa wito kwa maafisa wa utawala wa serikali kuu kusimamia kwa karibu mipango na miradi ya serikali katika maeneo yao ya utawala. 

Gachagua amesema maafisa hao ni wawakilishi wa Rais William Ruto mashinani na ni lazima wachukue jukumu la kuhakikisha miradi hiyo haikwami wakitazama bali inatekelezwa kama ilivyopangwa.

“Ni wajibu wenu kulinda hadhi ya Rais. Wakati Rais amezindua mradi na mkandarasi anautelekeza baada ya wiki moja, hadhi ya Rais inatiliwa shaka. Mna wajibu wa kuhakikisha hilo halifanyiki na likifanyika, ni sharti mmtaarifu Katibu na Waziri husika ili hatua stahiki ichukuliwe,” alisema Naibu Rais.

Aliyasema hayo katika taasisi ya mafunzo ya serikali katika eneo la Lower Kabete alipoandamana na Rais Ruto alipowahutubia maafisa wa utawala kutoka kote nchini.

Kulingana na Naibu Rais, ni wajibu wa maafisa hao kuwa makini na kufuatilia hatua ya utekelezaji wa miradi hiyo ili kufikiwa haraka kwa malengo yaliyokusudiwa.

“Nyinyi ni macho ya Rais mashinani. Wakati miradi ya serikali haiendelei vizuri na mnasalia kimya, mtakuwa mmemwangusha Rais.”

Martin Mwanje & DPCS
+ posts
Share This Article