Maafisa wa usalama wapelekwa kudumisha amani Tana River

Tom Mathinji
1 Min Read
Inspekta Jenerali wa polisi Douglas Kanja.

Inspekta Jenerali wa Polisi Douglas Kanja amesema  maafisa wa asasi za usalama wamepelekwa katika kaunti ya Tana River kudumisha amani, siku chache baada ya eneo hilo kukumbwa na visa vya utovu wa usalama.

Juma lililopita watu wanane walifariki baada ya jamii mbili kukabiliana kuhusu kile kilichotajwa kuwa mzozo wa ardhi.

Kupitia kwa taarifa, Mkuu huyo wa polisi alisema hali ya usalama imeimarishwa huku maafisa wa huduma ya taifa ya polisi (NPS), maafisi wa vikosi vya ulinzi (KDF) na wale wa upelelezi wa makosa ya jinai (DCI) wakipelekwa katika eneo hilo.

“Kwa sasa hali imedhibitiwa, na tunatoa wito kwa jamii za eneo hilo kuendelea kudumisha amani,” alisema Kanja kupitia kwa taarifa.

Kulingana na Kanja idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai DCI, imeanzisha uchunguzi kuhusiana na ghasia hizo zilizosababisha maafa hayo.

Alitoa wito kwa wananchi kuvijulisha vyombo vya usalama kuhusu matukio yanayoweza kuvuruga amani na kuhatarisha maisha.

Share This Article