Maafisa wa usalama Laikipia watakiwa kukomesha ukosefu wa usalama

Naibu Rais Rigathi Gachagua ameelekeza maafisa wa usalama katika kaunti ya Laikipia kukomesha visa vya ukosefu wa usalama katika eneo hilo akionya kwamba uzembe hautavumiliwa.

Akizungumza katika kanisa katoliki la Holy Family Ng’arua baada ya kuhudhuria misa na mchango, Gachagua alisema uwezo wa kimaendeleo wa eneo hilo unalemazwa na ukosefu wa usalama na serikali ya Rais Ruto haiwezi kubalia hali hiyo kuendelea.

Kulingana naye, Rais Ruto ni sharti atimize ahadi alizotoa wakati wa kampeni mwaka 2022 hasa ile ya kutokomeza ukosefu wa usalama.

Kiongozi huyo anasema haoni kinachozuia maafisa wa usalama wa eneo hilo kukomesha uvamizi dhidi ya raia huku akikumbuka aliwahi kuhudumu kama mkuu wa wilaya katika eneo la Ng’arua mwaka 1998.

Wakati huo, vita vya kikabila vilikuwa vinashuhudiwa pamoja na uvamizi wa majambazi lakini alishirikiana na maafisa wa usalama na jamii kurejesha amani.

Alisema watu wa eneo hilo sharti wafurahie usalama wao na maafisa wazembe hawatahamishiwa kwingine.

Akihutubia raia katika soko la Matuiku, Gachagua alielekeza kamishna wa kaunti Joseph Kanyiri na kamanda wa polisi wa kaunti hiyo ya Laikipia wawasake na kuwakamata wahalifu wanaosumbua wananchi.

Kando na suala la usalama, Gachagua alisema kwamba serikali inawekeza katika kilimo cha unyunyiziaji mashamba maji na maendeleo mangine ya miundombinu ili kuafikia uwezo kamili wa eneo hilo kijamii na kiuchumi.

Alitoa hakikisho la serikali kujitolea kumaliza mizozo kati ya binadamu na wanyamapori ili kuepusha vifo na uharibifu wa mali kufuatia wanyama wanaorandaranda kutoka kwa mbuga ya Laikipia.

Gachagua aliwataka wabunge kurekebisha sheria ili kutoa fursa kwa maafisa wa huduma ya taifa ya polisi kusaidia walinzi wa wanyamapori katika kudhibiti wanyama hao.

Aligusia pombe haramu na dawa za kulevya ambapo alielekeza viongozi wa eneo hilo kumakinika katika vita dhidi ya vitu hivyo.

Viongozi waliokuwa wameandamana na naibu rais waliahidi kuwajibika zaidi ili kuunga mkono serikali inapotekeleza majukumu yake.

Website |  + posts
Share This Article