Maafisa wa Uganda walaumiwa kwa kudhulumu waandamanaji

Marion Bosire
2 Min Read

Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch (HRW) limelaumu maafisa wa serikali ya Uganda kwa kile kinachotajwa kuwa kudhulumu, kukamata na kuchapa wanaharakati na watu wengine ambao walikuwa wakiandamana kupinga mradi mkubwa wa mafuta katika eneo la Afrika Mashariki unaoongozwa na kampuni ya Ufaransa ya Total Energies.

Mradi huo wa dola bilioni 10 wa kampuni ya Total Energies na ile ya China National Ofshore Oil Corporation wa kuboresha maeneo ya kuchimba mafuta nchini Uganda ulisifiwa na Rais wa Uganda Yoweri Museveni ambaye aliutaja kuwa wa maana kiuchumi lakini umepingwa na wanaharakati wa haki na makundi ya kulinda mazingira.

Hatua za kisheria zimechukuliwa dhidi ya mradi huo nchini Ufaransa na bunge la nchi hiyo limeonyesha kutoridhika na hatua ya kuzuilia watetezi wa mazingira na kufurushwa kwa watu kutoka ardhi husika bila fidia faafu.

Mradi huo unajumuisha kuchimbwa kwa visima vya mafuta 400 katika eneo la mbuga ya kitaifa ya Murchison Falls na bomba la kilomita 1,445 la kusafirisha mafuta hayo hadi bandari ya Tanga nchini Tanzania.

Kampuni ya Total Energies inasema waliofurushwa na mradi huo wamefidiwa kwa njia inayofaa na kwamba hatua zimechukuliwa za kulinda mazingira.

Shirika la HRW lilihoji watu 31 nchini Uganda na Tanzania kati ya mwezi Machi na Septemba 2023, wakiwemo wanaharakati 21 na wengi wao walisema wamekumbwa na vitisho,unyanyasaji na kukamatwa bila makosa.

HRW ilitaka mradi huo usitishwe mwezi Julai mwaka huu kutokana na athari zake kwa mazingira na kwa watu lakini Rais Museveni ameapa kuendelea nao.

Share This Article