Makamu wa Rais wa Equatorial Guinea Teodoro Nguema Obiang Mangue ameonya wafanyakazi wa serikali dhidi ya kufanya mapenzi kazini akisema watachukuliwa hatua kali.
Onyo hili linajiri saa chache baada ya kuvujishwa kwa video nyingi zinazomhusisha Baltasar Ebang Engonga anayeonekana akishiriki tendo la ndoa na mamia ya wanawake, wakiwemo wake za viongozi mbalimbali nchini humo.
Engonga anaongoza shirika la kitaifa la uchunguzi wa kifedha na ni jamaa wa Rais wa nchi hiyo Teodoro Obiang Nguema Mbasogo.
Kupitia ukurasa wake wa Facebook, Engonga alisema kwamba amehuzunika sana huku akichapisha picha ya familia yake akisema familia ni kila kitu.
Makamu wa Rais Teodoro Obiang Mangue anasema afisa yeyote wa serikali atakayepatikana akijihusisha katika mapenzi kazini atasimamishwa kazi kwa kukiuka maadili ya kazi.
Kiongozi huyo sasa ameamuru kuwekwa kwa kamera za CCTV kwenye afisi za serikali kama vile mahakama na hata za wizara kama njia ya kukabiliana na visa hivyo.
Mangue alipendekeza pia uchunguzi kuhusu suala hilo.
Engonga alikamatwa wiki jana kuhusiana na madai ya ufisadi kabla ya video hizo kuvuja na kusambazwa kote mitandaoni.
Afisa mkuu anayesimamia mashtaka ya umma nchini Equatorial Guinea Anatolio Nzang Nguema alitangaza kwamba uchunguzi utatekelezwa na iwapo Engonga atapatikana na ugonjwa wa zinaa, atashtakiwa kwa kuhatarisha afya ya umma.